Kisu Moyoni; Usaliti mgongoni mwangu. [Sehemu ya kwanza]

Hakua anaamini kile anachokiona, maumivu kifuani yalimchoma kama mwiba, akahisi kifua kizito huku mapigo ya moyo wake yakiongezeka, jas...



Hakua anaamini kile anachokiona, maumivu kifuani yalimchoma kama mwiba, akahisi kifua kizito huku mapigo ya moyo wake yakiongezeka, jasho jembamba likaanza kumbubujika huku mikono ikiwa inamtetemeka, alikua anatetemeka sio kwa kile alichokiona ila kwa kiasi ambacho haamini kama kweli yametokea, alipigwa na bumbu wazi, hata sehemu aliokua akielekea hapakua pa muhimu tena, akajisogeza pembeni kidogo mwa bara bara na kujiegesha juu ya gogo lililokua karibu kwa jinsi alivyokua ameishiwa nguvu miguuni, akavuta pumzi na kuishika vizuri simu yake ili kuisoma vizuri meseji.

Alijaribu kurudisha akili nyuma, akijiuliza na kufunua kila kumbukumbu iliyokichwani mwake, ni kitu gani hasa alichokua amekosea kukifanya ndani ya wiki tano zilizopita mpaka barua yake ya kusitishwa kazi iwe imewasilishwa ofisini kwake, alijaribu kurudia rudia kuisoma hio meseji iliyotokea kwa bosi wake bwana Benedicto akimjulisha kwa meseji ujio wa barua yake iliyotokea makao makuu na kumsihi asitishe likizo na arudi ofisini haraka iwezekanavyo ili aweze kukabidhi nyaraka za ofisi na kushughulikia mafao yake, likizo aliyokua ameiyomba ya siku tatu kufuatilia kesi iliyokua mahakamani ya taraka mke wake aliyokua anaitaka, kesi ambayo ilikua inatakiwa itolewe maamuzi siku hio hio na ilikua inatakiwa ianze nusu saa tokea alipoondoka gesti aliyokua amepanga mnamo saa mbili asubuhi, alishitushwa na joto la miale ya jua kutoka kwenye mawazo yake ambayo yalikuwa hayana jibu la nini kimesababisha majanga ya kufutwa kazi, alisimama na kuangalia majira kwenye saa yake ya mkononi ambayo ilikua inasoma saa tatu na dakika kumi na moja.

Alikurupuka na kuanza kukimbia ajaribu kuwahi hukumu kabla haijatolewa, ilimchukua dakika kumi zingine kutokea pale alipokua amekaa mpaka kufikia eneo la mahakama, alifungua mlango wa mahakama kwa nguvu huku akihema kutokana na mbio alizokimbia kuwahi kesi na kukuta mahakama tayari imeshafanya uwamuzi, alitembea taratibu akiwa anaelekea usawa aliokuwa wakili wake ambaye alikua anamuangalia kwa jicho la ukali huku sura yake ikiwa na huruma na masikitiko makubwa, sura hiyo ya wakili wake ilimfanya achanganyikiwe zaidi, nguvu ziliendelea kumuishia zaidi na kufanya agongane na watu aliokuwa anapishana nao waliokuwa wakitoka nje ya mahakama baada ya kesi hio kumalizwa kusikilizwa huku wengine wakiwa wanamtazama na kuonyesheana vidole, alifika na kukaa kwenye kiti alichotakiwa awe amekaa wakati kesi yake ilipokua inasikilizwa, wakili wake aliyekua amesimama alijongea karibu na kukaa kiti kilichokua pembeni yake, akavuta pumzi kwa hisia, huku akionekana kutafuta maneno ya kumwambia, alimwangalia kinywa kikiwa wazi, akameza mate na kuongea,

"John, ulilala wapi usiku wa kuamkia leo?"

"Nililala gesti mtaa wa Ghana, pale High way guest house, unajua nisingeweza kwendwa nyumbani wakati mimi na mama venessa hatuelewani mpaka kesi ipo hapa na wewe ndo wakili wangu, achana na nilipolala niambie kuhusiana na kesi wakili Sebastiani!".

Wakili; "Kesi imeshindikana kusikilizwa!".

John; "kwanini?"

Wakili; "Nyote wawili hamkutokea, mahakama imefanya maamuzi na imehailisha kesi kwa muda usiojulikana kutokana na mwingilio wa jambo jingine lililotokea na kulipa muda jeshi la polisi kufanya upelelezi wa kina!".

John; "Jambo gani tena linaloweza kutokea wakati kilichopo ni maamuzi tu kupitishwa jinsi gani tutakavyo gawana mali na kusaini hizo karatasi za talaka, na imekuwaje mama venassa hajatokea?".

Wakili akashikwa na kigugumizi na kumwangalia John huku akiwa amekosa kitu cha kumjibu, akailegeza tai yake shingoni na kujikuna nywele zake huku akimwangalia John kwa tafakari ni kipi cha kumjibu huku akisita kuongea, John akageuka na kugeza kiti ili akae usawa wa wakili akiwa na husuda ya kusikia kile wakili atakachokiongea, wakili akavuta pumzi tena na kuanza kuongea.

Wakati John na wakili wake sebastiani wakiwa wanaendelea kuongea, watu watatu waliokuwa wamevaa sare ya polisi waliwasogelea kutoka nyuma, na kumgusa John begani, John akageuka na kumfanya wakili Sebastiani naye kugeuka, wakaanza kujitambulisha.

Polisi wa kwanza; "Mie naitwa Afande Joakimu, huyu kushoto ni afande Amosi na huyu mwingine ni afande Butaigwa, ni maafisa polisi kutoka kituo cha kati cha kirumba".

Afande Joakimu akatoa kitambulisho chake cha kazi na kumuonyesha John, wakili Sebastiani akakipokea na kukisoma kwa ukaribu zaidi, na wenzake nao afande Amosi na Butaigwa nao wakavitoa vya kwao, John akapokea cha Butaigwa na kuanza kukisoma, wote kwa pamoja wakili Sebastiani na John wakawarudishia baada ya kumaliza kuvisoma.

Afande Joakimu akamuuliza John, "Unaitwa nani ndugu?''.
John akamjibu huku akimwangalia yule afande Joakimu machoni kwa tamaa ya ufahamu ni nini wanachokihitaji na kipi wanachokifuatilia kwake.

"Naitwa John Alexander".

Afande Joakimu; Bwana John upo chini ya ulinzi kwa tuhuma za kumuua mkeo, Anna Maiko John aliekutwa amekufa leo asubuhi nyumbani kwako akiwa na majeraha ya kisu tumboni, kutokana na kutoelewana kati yako na yeye, pamoja na kesi iliyopo na inayoendelea mahakamani ya talaka, we ni mtuhumiwa namba moja, kwahio tunakuitaji tuende wote kituoni.

John alipigwa na mshituko na bumbu wazi na kugeuka na kumwangalia wakili, afande Joakim akaendelea kuongea, Tunaomba uinuke ili tuweze kuelekea kituoni.

Wakili Sebastiani akamwangalia John na kumwambia akifikishwa kituoni asiongee kitu mpaka hapo yeye atakapowasili, anachukuwa vitu vyake ofisini anavyovihitaji watakutana kituoni ndani ya muda mfupi, Sebastiani akamgeukia afande Joakim na kumwambia, "Mimi ni mwanasheria wake naomba asihojiwe mpaka niwepo".

Afande Joakimu akatikisa kichwa kuonyesha kukubaliana na wakili Sebastiani kwa kile alichokua anakiongea, John akanyanyuka na afande Amosi akamsogelea na kumvalisha pingu na kumshikilia sehemu ya mkono wake wa kushoto na wote kwa pamoja wakaelekea nje ya mahakama na kumpandisha John nyuma ya gari aina ya difenda lililokuwa limepakiwa karibu kabisa na mlango wa mahakama, naye pia akapanda akifuatiwa na afande Butaigwa wakati afande Joakimu yeye akapanda mbele pembeni mwa dereva, gari ikawashwa na safari ya kuelekea kituoni ikaanza.

Wakati gari likiwa linaendelea na safari, John alikua amekaa kwa kujikunyata, huku mikono yake akiwa ameiweka usawa wa tumbo na kuibana na mapaja kana kwamba alikuwa anahisi baridi kali, hakuwa anajua ni nini cha kufikilia, mawazo yalikuwa mengi kiasi cha kutojua mahali pa kuyaanzia kuyawaza, wazo moja lililokuwa na nguvu kuliko yote ni kwanini mama Venassa ameuwawa, ni nani aliyemuuwa?, alitamani kuwauliza maafande jinsi walivyoikuta nyumba yake iwapo kuna kitu chochote kilikuwa kimeibiwa ila kwa macho waliokuwa wakimuangalia ya kumtuhumu yalimfanya ashindwe hata kufungua kinywa chake, afande Butaigwa huku akimkazia macho John akajisogeza kidogo na kukaa usawa mzuri na kuanza kumuhoji John, "Unajua ni vizuri ukawa mkweli na muwazi ni nini na sababu gani iliyokupelekea kumuuwa mkeo, unaonekana ni mtu nadhifu na mpole, ilikuwa sababu ya mali?".

Kwa mawazo John aliyokuwa nayo hakuweza hata kumsikia kile Butaigwa alichomuuliza, Butaigwa akachukia akawa amehisi John amemfanyia kiburi, akampiga kofi zito la kushitukiza upande wa wa kushoto wa paji la uso ambalo lilimpeleka chini na kumfanya John kuangukia mkono wake wa kulia kutoka sehemu alipokua amekaa, afande Amosi akaingilia kati na kumpoza Butaigwa kwa kumuambia "muache akifika kituoni lazima ataongea yale aliyoyafanya!", kwa kofi alilopigwa John lilikuwa limemkuta katika mazingira ambayo halikua halitegemei kwa mawazo yaliokuwa yamemzingira kichwa chake, alijaribu kuamka lakini alikuwa anajisikia kizunguzungu na mlio masikioni, afande Butaigwa akamkanyaga John eneo la ubavu kwa nguvu na kumuamuru aamke na kukaa vizuri eneo alilokua amekaa awali, akajikokota na kuamka kabla hajafikia sehemu alilokua amekaa difenda lilikata kona na kusimama.

Difenda lilikua limefika kituoni, afande Amosi akamshika mkono na kumsaidia kumshusha na kuingia naye ndani ya kituo huku afande Butaigwa akiwa kwa nyuma akifuatiwa na afande Joakimu na kuelekea moja kwa moja kwenye chumba cha maelezo, afande Joakimu akamuamuru John akae chini sakafuni pembeni kidogo ya meza na maafande wote wakavuta kiti na kukaa kwa kuizunguka hio meza, afande Amosi akavuta droo na kutoa karatasi na kuanza kuzipanga huku akiwa anaandika vitu flani kwenye karatasi hizo, John alikuwa anatetemeka kwa hofu na uso wake ulikuwa umejawa huzuni nyingi, akili ilikuwa haifanyi kazi vizuri tena, mashaka yalikuwa yameutanda moyo wake na akawa na woga na wale maafande kutokana na vitu afande Butaigwa alivyomfanyia ndani ya gari, Afande Amosi akamshitu John kwa sauti, "Wewe, unaitwa nani?'',

"Naitwa John Alexander"

Afande Joakimu; "taja majina yako matatu kwa pamoja!"

John akajibu kwa unyenyekevu mkubwa huku akimwangalia afande Amosi kwa upole, "naitwa John Alexander Nyamuhanga".

Afande Amosi; "kabila yako?",

John; "Mkurya".

Afande Joakimu akamuangalia Butaigwa huku akitabasamu, "Butaigwa, wa kwenu huyu!", aaah wapi, mi sina ukoo na wauwaji, Butaigwa akamjibu Joakimu huku akimwangalia John kwa hasira, walipokutanisha macho na John, John akaangalia pembeni.

Afande Amosi akaendelea kumuhoji John, "Umri wako?".

John; "Miaka 31"

Afande Amosi; "Dini yako?"

John; "Romani Katoliki"

Afande Amosi; "Kazi yako?"

John; "Muhasibu benki kuu ya tanzania tawi la mwanza".

Afande Joakimu, Butaigwa na Amosi waliangaliana kwa pamoja kwa kustaajabu, "Huyu naona anatutania, anahisi labda kuwa wapelelezi ni jambo jepesi na rahisi sana!", Afande Butaigwa aliongea huku akimgeuzia macho John, "unasema unafanya kazi wapi?".

John alisita kuongea kutokana na macho waliokua wanamtazama ya ukali, kabla hajajibu afande Joakimu akamsogelea na kumfungua pingu alizokua amefungwa mikononi kwa mbele na kuchukua mikono ya John na kuipeleka kwa nyuma na kumfunga pingu mikononi nyuma ya mgongo, afande Butaigwa akatoa rungu pembeni ya meza karibu na kona ya hicho chumba, akamwambia John asome lile rungu lilivyo andikwa, John akiwa na wasi wasi mwingi na woga pamoja na hofu alilisoma kimya kimya na kumuangalia afande butaigwa na kumwambia "limeandikwa mama mkanye mwanao!".

Afande Joakimu akamshika shati John kwenye kola upande wa nyuma na kumburuza kwelekea pembeni kidogo kwenye nafasi ya wazi karibu na kabati iliyokuwa imejaa mafaili, afande Amosi naye akaamka na kusogea kwenye mrango wa chumba na kuufunga na kusogea mahali John alipokua, Butaigwa akafungua kabati na kuchukua kamba naye akamsogelea John na kuanza kumfunga kamba miguuni.

John akajawa hofu kubwa na kufumba macho na kuanza kusali, "baba yetu uliembiguni, jina lako litukuzwe ufalm...!", afande Butaigwa alichukua lile rungu na kumpiga nalo John eneo la goti la kulia, John akapiga kelele kwa maumivu makali, "Ulimuua mkeo?", afande Joakimu akamuuliza John kwa sauti ya ukali, huku afande Amosi akicheka na kusema "wewe utatuambia tu, tumeshakutana na majambazi gaidi kuliko wewe na wakatuambia siraha wanapozificha sembuse wewe!".

"Unaonekana ni mwongo sana, tumeshakufuatilia toka asubuhi ulipokimbia nyumbani kwako, tukaenda kazini kwako tukaambiwa umeshaachishwa kazi halafu sasa hivi unatuambia unafanya kazi benki kuu, unatuona unatuzidi akili eehe?", Butaigwa aliongea kwa kufoka na kumpiga kofi zito John, kwa maumivu aliyokuwa anajisikia John alikua anaomba mungu wakili sebastiani atokee aje amsaidie, rungu jingine tena lilitua kwenye goti la mguu wa kushoto na kumfanya John aongeze tena kilio cha maumivu huku akitaja kwa kurudia rudia "mimi sijamuuwa mke wangu, mimi sijamuuwa mke wangu!", maafande walionekana dhahiri kutosadiki maneno aliyokua akiyanena John, na waliendelea na kumuongezea kipigo sehemu za maungio ya viungo na kumfanya John kunyongonyea kabisa.

Ngo' ngo' ngo' ngo!, ulikuwa mlio wa hodi mlangoni, uliomuokoa John na kufanya maafande wasitishe zoezi walilokuwa nalo, Afande Amosi akausogelea mlango na kutaka kuufungua, "Acha kwanza!", ni sauti ya afande Joakimu ikimuamuru afande Amosi asubiri kwanza wakati afande Butaigwa akimfungua John kamba alizokua amefungwa huku yeye akilirudisha rungu eneo lilipokuwa awali, walipoweka kila kitu sehemu yake wakamuamuru John asimame, John akiwa bado kwenye maumivu makali alijaribu kusimama lakini akashindwa na kuanguka chini kama mzigo, afande Butaigwa akamsogelea John na kumuongeza kibao kingine cha nguvu na kumuamuru John asimame na aanze kuruka ruka, John akasimama huku usoni akionyesha yupo kwenye maumivu makali na kuanza kuruka ruka kwa mguu mmoja wa kulia huku wa kushoto akiwa hawezi kuutumia vizuri.

Maumivu yalimshinda John, jasho lilimmiminika kama maji huku puwa zikiwa zinatokwa makamasi mfululizo ya maji maji, macho yalikuwa mekundu kwa machozi na maumivu anayoyasikia, alianguka kama mzigo kwa mara ya pili na hakuwa na nguvu tena za kunyanyuka, afande Amosi alifungua mlango na kukuta tayari mgongaji ameshaondoka, ikabidi atoke na kuelekea kaunta kuulizia zaidi ni nani aliyekuwa anagonga, afande Joakimu na Butaigwa waliendelea kumuhoji John, "Kaa vizuri!", John aliamka na kukalia makalio, akavuta shati lake na kujifuta jasho na makamasi yaliokuwa yakimtoka, "tukiangalia kwa uelewa, iwapo mkeo akiwa amekufa kama hivi, ni nani anayefaidika zaidi na kifo chake, maana kugawana mali kwenye taraka kutakuwa hamna tena, sio wewe?", afande Joakimu aliendelea kumuhoji John, John alitikisa kichwa kuashilia kukubali. "Usitikise kichwa, sema ndio au hapana!", afande Butaigwa alifoka, "Ndio", John akajibu haraka haraka, sasa tuambie iwapo hukumuuwa wewe ni nani ambaye alikuwa na kisa na mkeo kiasi cha kumuuwa?, afande Joakimu aliendelea, "hakuna aliyekuwa na kisa naye kwa mimi ninavyofahamu", John akajibu huku akiangalia chini.

"Tukiwa tunakuuliza maswali jibu huku unatuangalia, ili tukujue ukiwa unatudanganya", Butaigwa alifoka tena, "Uliondoka nyumbani saa ngapi?", afande Joakimu aliendelea kumuhoji John, "sijafika kabisa nyumbani tokea siku tatu zilizopita", John alijibu, mlango ulifunguliwa ghafla na afande Amosi akaingia "mkuu anatutaka twende Ghana kuna tukio!", afande Joakimu akafunga jarada alilokuwa nalo na kumwambia afande Butaigwa ampeleke John lokapu, Butaigwa akamchukua John huku akichechemea mpaka kaunta, akaandika maelezo kwenye kitabu cha taarifa akamwambia John avuwe viatu na mkanda, akamsachi alipo lidhika akampeleka moja kwa moja sero.

Tokea asubuhi askari walipofika na kumkosa John eneo la mahakama, Sebastiani hakukubaliana kabisa na tuhuma ambazo John zimemkuta, kwa muda wote anaomfahamu John na mambo yote waliopitia wakiwa pamoja hakuweza kabisa kuamini kama John anaweza kufanya kitendo cha namna hio, baada ya polisi kumchukua John pale mahakamani, Sebastiani alielekea ofisini kwake na kuchukua mkoba wake wa kazi na kuanza safari ya kuelekea nyumbani kwa John tukio lilipofanyikia ili aweze kufanya uchunguzi wake binafsi.

Alipofika nyumbani kwa John, Kitangiri mtaa wa mediko hakutaka kuingia ndani na gari japo geti lilikuwa wazi, alipaki gari lake nje na kushuka, alitaka kuwa makini ili aweze kulichunguza eneo la tukio kwa ufasaha zaidi japo polisi tayari walikuwa wameshafanya hivyo, moyoni alijua yeye ndo mtu wa mwisho anayeweza kumsaidia John, aliingia ndani ya geti na kutembea taratibu huku akichunguza mazingira ya nje, akafika kwenye mlango mkuu wa kuingia ndani ya nyumba, akaufungua nakukuta ulikuwa wazi akaanza kuchunguza iwapo kitasa kimebomolewa kama mtu aliingia kwa kutumia nguvu ila kitasa kilikuwa salama, akaangalia sebure iwapo kulikua na kitu chochote ambacho hakikua sehemu yake, ilimchukua zaidi ya saa moja kuchunguza sebure pekee ila hamna chochote alichoweza kuambulia, aliamua kuhamia kwenye chumba sehemu tukio lilipotakea, japo mwili wa marehemu ulikuwa tayari umeshachukuliwa ila polisi walikuwa wameweka alama za utambuzi kwa jinsi walivyokuwa wamefanya uchunguzi wao, alijaribu kufuatilia mazingira ya chumba kwa makini ila hamna kitu kipya alichokiaona, ikambidi wakili sebastiani aondoke kuelekea mtaa wa Ghana kwenye gesti ya Highway Guest House ambapo John alimwambia alikuwa amelala huko usiku mzima wa kuamkia siku hio.

Alipofika Ghana pale high way guest house alishangazwa na umati wa watu uliokuwa umekusanyika, polisi walikuwa kila sehemu, akapunguza kasi ya gari lake huku akiangaza huku na huko sehemu ya kupaki, akakata kona taratibu na kupaki pembeni kidogo karibu kabisa na bango la Highway guesti house, alishuka na kujongea karibu ili aweje kujua ni nini kilichotokea hadi kuwepo umati mkubwa wa watu kiasi hicho, alisimama kwa dakika kadhaa huku akiangaza huku na kule aweze kuelewa ni nini kinachoendelea, pembeni alimwona mwanamke mmoja aliyekuwa amevalia kanga huku nyingine kaifunga kifuani akiongea kwa mbwembwe na akionyesha dhahiri hali ya kutambua kila kitu kinachoendelea mahali pale, alikua akiwaadithia kikundi cha watu waliokuwa wamemzunguka kile kilichotokea huku akirusha mikono yake huku na kule, alisogea taratibu na kusimama karibu yake na kujaribu kutega sikio ila hakuweza kuelewa kile kinachozungumziwa, alimwacha amalize na kumuuliza tena ni nini kilichokua kinaendelea, "samahani mama, ni nini kinachoendelea mahali hapa?", "kuna mtu amejeruhiwa vibaya sana humo ndani, muhudumu wa usafi alienda kufanya usafi kwenye chumba kimoja cha gesti na kukuta damu nyingi sana, ilibidi apige kelele na meneja wa hii gesti akapiga simu polisi ndo wako ndani wanaendelea na uchunguzi, nadhani atapitishwa hapa sasa hivi we subiri uone!", yule mama alimjibu akiwa na shauku kubwa, huku macho yake ya udadisi yakiendelea kuangalia mlango wa gesti kwa hamu kubwa.

Wakili sebastiani alijipenyeza taratibu kwenye umati wa watu kuelekea kwenye mlango mkuu wa jengo hilo, kabla hajafika mbali alimuona kwa umbali afande Joakimu, "afande Joakimu!", alijikuta amepaza sauti kumuita afande Joakimu huku akimpungia mkono kuonyesha mahali alipo, afande Joakimu aligeuka na kuangaza macho usawa wa sauti ilipotokea, kwa mbali naye alimuona Sebastiani na kuanza kutembea kumfata mahali alipo, alipomfikia sebastiani alionyesha wazi kushitushwa na uwepo wa sebastiani mahali pale, "unatafuta nini mahali hapa?", bila kumsalimu au kumjulia hali afande Joakimu alimuuliza wakili Sebastiani kwa sauti ya ukali, Sebastiani alishitushwa na hali aliokuwa anaionyesha afande Joakimu, "kwani kuna kosa mie kuwa mazingira haya?", Sebastiani alimjibu Joakimu huku akimwangalia machoni kwa jicho la udadisi, "nijibu kwanza upo mtaa huu, gesti hii unatafuta nini?" afande joakimu aliendelea kuonyesha msimamo wake wa kutaka kujua wakili Sebastiani yupo pale anatafuta nini.

"Nipo nafanya uchunguzi binafsi wa tuhuma alizotuhumiwa John na alinielezea asubuhi alilala hapa, nimetokea kwake sasa ndo nilikuwa napita hapa kukamilisha uchunguzi wangu!".

Sebastiani alimbidi awe mpole na kumjibu kile alichoulizwa,

"Kunanini mpaka unakuwa unaushangaa uwepo wangu hapa?",

"Jamaa yako alizania hatutompata eehe?, chumba namba tatu wakati muhudumu kaingia asubuhi kufanya usafi kakuta kina nguo za kiume zilizojaa damu na kisu pembeni yake, tukaenda kucheki kwenye kitabu chwa wageni kuangalia ni nani aliyekuwa amekikodisha, unajua ni nani?", Joakimu aliuliza swali huku akicheka kicheko cha kuridhika na kuonyesha dhahiri anamkebehi wakili Sebastiani,

Wakili Sebastiani aliishiwa nguvu, tumbo likamuunguruma na kuhisi kupatwa na kuhara, kimoyo moyo alimuomba mungu isiwe kama anavyofikilia kichwani mwake, alimwangalia afande Joakimu kwa jicho la upole, afande Joakimu aliona jinsi Sebastiani alivyonywea, "najua unampenda sana jamaa yako, ila hayupo jinsi ulivyokua unamfikiria wewe, kidhibiti tunacho na tumekipeleka kwa wachunguzi kumalizia utaratibu na sasa hivi hana pa kutokea, waambie ndugu zake waje wamuone kwa mara ya mwisho maana hawatamuona kwa muda mrefu sana!", afande Joakimu aliongea kwa kujiamini na sura yake ikionyesha hali ya ushindi mkubwa, aligeuka na kuondoka huku akimwacha Sebastiani kaishiwa nguvu kutokana nahabari alizompatia.

Jua la saa saba liliendelea kumchoma Sebastiani aliyekuwa amepigwa na butwaa zaidi ya dakika ishilini tokea alipoachwa na afande Joakimu, alianza kutembea kwa kujivuta taratibu kuelekea kwenye gari yake, hakua anaamini kile alichoambiwa, kuna kitu moyoni bado kilikua hakikubaliani na yale yote anayoyaona na kusikia kuhusu John, alivuta kumbukumbu zake nyuma na kuanza kukumbuka mara ya kwanza alipokutana na John kidato cha kwanza shule ya sekondari Thaqaafa, kipindi chote cha shule walipokua wakisoma na kucheza pamoja, walipofaulu kwa pamoja na kupelekwa Kigosera High School kule wilaya ya mbinga mkoa wa Iringa, jinsi walivyoishi pamoja na jinsi John alivyokuwa mpole na rafiki mzuri kwake, alipolikaribia kabisa gari alijikuta akijikwaa na kuanguka chini kutokana na mawazo aliyokuwa nayo yaliyomsababisha kutokuangalia pale anapokanyaga, aliamka taratibu bila kujipangusa vumbi alilokua nalo na kufungua mlango wa gari na kujitupia kwenye kiti cha dereva huku macho yakiwa mekundu yaliolengwa na machozi kwa mbali, alijipikicha macho na kuchukua simu yake na kufungua orodha ya majina, akachagua jina moja kisha akabonyeza kitufe cha kupigia simu na simu yake ikaanza kuita.

Alijikongoja huku akichechemea taratibu, macho yake yakiwa mekundu na uso wake kukunjamana kwa maumivu anayoyasikia katika kila mfupa alionao mwilini mwake, aliangalia huku na kule kutafuta eneo litakalo mfaa kulala chini, watuhumiwa wengine walimshangaa kwa michilizi ya damu iliyokuwepo magotini, mmoja aliamka na kumsaidia kutembea kwa kumshika mkono mmoja wa kushoto na kumuingiza kwenye chumba cha kwanza kati ya vyumba vitatu vilivyokuwemo humo lokapu na kumuweka juu ya kitanda cha zege, zege lililojionyesha asili lilikuwa la kipindi cha wakoloni, John alijaribu kijilaza ila maumivu ndivyo yalivyokua yakiongezeka kila anapojitingisha, "naitwa Shija, umekuwaje mbona wakati unaingia tumekuona kupitia kwenye mlango wa nondo za lokapu ukiwa mzima?", kijana aliyemsaidia kumshika mkono wakati wa kutembea alimuuliza, "kaka Shija samahani najua unataka ufahamu yalionikuta, ila nakuomba unipe mda nipumzike kidogo haya maumivu yatulie kidogo na kupumzisha akili ili tuweze kuongea kwa uzuri zaidi!", John alimjibu huku sauti yake ikiwa inakwama kwa kwikwi za hasira na maumivu aliyokuwa nayo.

Alijaribu kufumba macho usingizi umchukuwe ili aihame hii dunia na siku iliyokua inamuendea vibaya kwake ila ilishindikana, hakuwa na cha kuwaza wakati dhahiri alijua hajafanya vitu vyote hivi vinavyotuhumiwa na kuwekwa mbele yake, alimfikilia mtoto wake Vennasa, alivyo mdogo wa miaka sita, japo alikua anajua mwanae yupo katika malezi mazuri kwa wakati huo katika shule ya kimataifa ya bodi inayoitwa Serengeti Internatinal School iliyopo Musoma mkoa wa Mara ambayo inamtunza vizuri, hofu yake ilikua ni ya maisha ya baadae ya mwanae Vennasa iwapo yeye akifungwa kifungo cha maisha, mawazo yake yalihama tena na kuanza kumfikilia mama yake venassa, jinsi walivyokutana naye alipokua anaanza kazi benki huku wakati huo John tayari alikua ana zaidi ya mwaka mmoja kazini, akafikilia tena mama Venasa jinsi ambavyo alianza kubadilika ghafla miezi minne iliyopita na kuanza kudai taraka, taraka ambayo imeleta mambo yote haya mpaka sasa yupo hapa alipo, taraka ambayo hakujua hata kisa cha kuidai kimetokea wapi, taraka ambayo alimsihi na kumbembeleza mke wake aachane nayo kwa sababu alikua anampenda na kumuhaidi kumpenda daima ambacho ndo kisa kikuu kilichomsababisha mkewe alete kesi mahakamani na kumfanya yeye kuhama nyumbani.



Itaendelea...

Hadithi hii ni ya kusadikika.

Imeandikwa na Lucas John.

COMMENTS

Jobstanzania
Name

Fasheni,3,Jua Zaidi,10,Mahusiano,19,Mazoezi,4,Mchezaji wa Mapenzi,22,Picha Maneno,14,Slider,6,Top Stories,12,WaulizeWanaume,3,
ltr
item
Kiumeni - WaulizeWanaume.: Kisu Moyoni; Usaliti mgongoni mwangu. [Sehemu ya kwanza]
Kisu Moyoni; Usaliti mgongoni mwangu. [Sehemu ya kwanza]
https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEggj9DnA0qZBDM4wssC343wwcOtcXPRWHQiOaM_kqiTz8Zf60cN3MDx7tvMb67inr2Xl_ytLu2EcRv8WM9ekFvua0ypG2Kz98Yi6SDz7W1TNX0LXHF-YAkKOCDfC6-LgLVPEOGE-ynfA9-K/s1600/Kisu+Moyoni+-+waulizewanaume..jpg
https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEggj9DnA0qZBDM4wssC343wwcOtcXPRWHQiOaM_kqiTz8Zf60cN3MDx7tvMb67inr2Xl_ytLu2EcRv8WM9ekFvua0ypG2Kz98Yi6SDz7W1TNX0LXHF-YAkKOCDfC6-LgLVPEOGE-ynfA9-K/s72-c/Kisu+Moyoni+-+waulizewanaume..jpg
Kiumeni - WaulizeWanaume.
https://waulizewanaume.blogspot.com/2014/06/kisu-moyoni-usaliti-mgongoni-mwangu.html
https://waulizewanaume.blogspot.com/
http://waulizewanaume.blogspot.com/
http://waulizewanaume.blogspot.com/2014/06/kisu-moyoni-usaliti-mgongoni-mwangu.html
true
5715942833127633596
UTF-8
Loaded All Posts Not found any posts VIEW ALL Readmore Reply Cancel reply Delete By Home PAGES POSTS View All RECOMMENDED FOR YOU LABEL ARCHIVE SEARCH ALL POSTS Not found any post match with your request Back Home Sunday Monday Tuesday Wednesday Thursday Friday Saturday Sun Mon Tue Wed Thu Fri Sat January February March April May June July August September October November December Jan Feb Mar Apr May Jun Jul Aug Sep Oct Nov Dec just now 1 minute ago $$1$$ minutes ago 1 hour ago $$1$$ hours ago Yesterday $$1$$ days ago $$1$$ weeks ago more than 5 weeks ago Followers Follow THIS CONTENT IS PREMIUM Please share to unlock Copy All Code Select All Code All codes were copied to your clipboard Can not copy the codes / texts, please press [CTRL]+[C] (or CMD+C with Mac) to copy